Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amekosoa vikali mifumo ya kawaida ya uwekezaji na ufadhili kutoka nje, akidai kuwa baadhi ya mifumo hiyo inaweza kuendeleza utegemezi wa kiuchumi wa nchi za Afrika.
Akizungumza mbele ya Wanafunzi, Wasomi na watunga sera, Traoré alieleza mtazamo wake kwamba mitaji kutoka kwa Wawekezaji wa kigeni inaweza kuwafaidisha zaidi Wawekezaji kuliko Wafanyakazi na uchumi wa ndani.
“Mwekezaji anapokuja kutoka nje akiwa na fedha zake, kwangu mimi huo ni aina ya utumwa. Ni kwa ajili ya kuwafanya ninyi mfanye kazi, lakini faida inakuwa yao.”
Kauli hiyo inaendana na msimamo wa serikali ya Traoré wa kutaka Burkina Faso kuongeza udhibiti wa ndani juu ya rasilimali na sekta zake muhimu za kiuchumi.
Traoré amesema nchi hiyo inapaswa kujenga mfumo wa uchumi unaolenga zaidi umiliki na manufaa ya ndani, badala ya kutegemea mifumo ya jadi ya ufadhili wa kimataifa.
Katika mwelekeo huo, amesema Burkina Faso inataka kudumisha umiliki wa asilimia 100 wa serikali katika sekta zitakazoainishwa kuwa za kimkakati, hatua inayoweza kubadilisha namna nchi hiyo inavyoshirikiana na Wawekezaji wa nje.
Msimamo wa Traoré unaonekana kuwa sehemu ya mabadiliko mapana ya sera za kiuchumi katika Burkina Faso na baadhi ya nchi za ukanda wa Sahel, ambako Viongozi wamekuwa wakisisitiza zaidi uhuru wa kiuchumi, umiliki wa rasilimali na kupunguza utegemezi wa mifumo ya kifedha kutoka nje.
Hata hivyo, Wakosoaji wa sera za aina hiyo huonya kwamba kupunguza nafasi ya mitaji ya kigeni kunaweza pia kuathiri upatikanaji wa fedha, teknolojia na utaalamu unaohitajika kwa maendeleo ya viwanda na miundombinu.
Kauli ya Traoré imeibua mjadala kuhusu swali kubwa: Je, uwekezaji wa kigeni ni chombo cha maendeleo kwa Afrika, au unaweza kuwa chanzo cha utegemezi wa kiuchumi?
