Waziri wa usalama wa ndani Marekani adai Ilhan Omar aliolewa na ndugu yake, aweza kukabiliwa na kufukuzwa Nchini.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani (DHS), Markwayne Mullin, amesema serikali ya Marekani inaendelea kuchunguza historia ya uhamiaji ya Mbunge wa Minnesota, Ilhan Omar, akidai kuwa huenda aliolewa na Mwanaume aliyekuwa ndugu yake kwa lengo la kumsaidia kuingia Marekani.
Mullin alitoa madai hayo Alhamisi Septemba 10, 2026 alipokuwa akizungumza na Mtangazaji wa kihafidhina Benny Johnson katika mkutano wa Chama cha Republican wa kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Dallas, Texas. Amesema uchunguzi huo bado unaendelea na kwamba endapo makosa ya uhamiaji yatathibitishwa, Omar anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo uwezekano wa kufukuzwa nchini Marekani .
Akielezea madai hayo, Mullin alisema: “Tunajua kwamba aliolewa na ndugu yake kwa lengo la kujaribu kumleta Marekani.”
Akaongeza: “Tunajua kwamba kwa sasa anaishi London.”
Mullin alikuwa akirejea Ahmed Nur Said Elmi, Raia wa Uingereza ambaye Omar alifunga naye ndoa mwaka 2009. Hata hivyo, madai kwamba Elmi ni ndugu wa Omar hayajathibitishwa hadharani, na hakuna ushahidi wa mwisho uliotolewa na serikali au Mahakama unaothibitisha kuwa ndoa hiyo ilikuwa sehemu ya ulaghai wa uhamiaji.
Waziri huyo pia alidokeza kuwa uchunguzi hauishii kwenye suala la ndoa pekee, bali unahusisha historia pana ya uhamiaji ya familia ya Omar.
“Huenda kukawa na zaidi ya hili; kuna suala zima la uhamiaji wa familia na huenda kukawa na shughuli nyingine zisizo halali zilizofanyika ili wao kuja Marekani hapo awali,” Mullin alisema.
Alisisitiza kwamba iwapo serikali itaamua kuchukua hatua dhidi ya Omar, hatua hiyo haitatokana na siasa bali ushahidi wa ukiukwaji wa sheria.
“Iwapo kweli tutaendeleza kesi, haitakuwa kesi ya kisiasa, bali itakuwa kesi halisi, kwa sababu walifanya mambo ambayo hayakuwa sahihi.”
Mullin pia alisema madai ya ulaghai wa uhamiaji hayana kikomo cha muda kwa namna ambavyo mamlaka zinaweza kuyachunguza, akisema endapo itathibitika kwamba mtu hakupaswa kuwepo Marekani tangu mwanzo, anaweza kuchukuliwa hatua za kumwondoa nchini Marekani.
“Hakuna muda wa mwisho kwa ulaghai wa uhamiaji. Ikiwa itathibitika kwamba mtu hakupaswa kuwa hapa tangu mwanzo, basi anaweza kufukuzwa.”
- Omar amekuwa akikanusha madai hayo.
Madai kwamba Omar alimuoa Elmi kwa lengo la kumsaidia katika masuala ya uhamiaji yamekuwepo kwa miaka kadhaa na yaliibuka kwa kiasi kikubwa wakati wa kampeni yake ya uchaguzi wa Bunge la jimbo la Minnesota mwaka 2016.
Omar, ambaye alifika Marekani akiwa Mkimbizi kutoka Somalia na baadaye akawa Raia wa Marekani mwaka 2000 akiwa na umri wa miaka 17, amekuwa akikanusha kwa nguvu madai kwamba Elmi ni ndugu yake.
Katika mahojiano na MPR News mwaka 2016, Omar alisema:
“Madai kwamba Ahmed Nur Said Elmi ni ndugu yangu ni ya kipuuzi na yanakera.”
Ofisi yake pia imekuwa ikipinga madai hayo, ikiyaita kuwa ya uongo na yenye msukumo wa kisiasa.
Kwa sasa, jambo muhimu ni kwamba madai ya Mullin yanaendelea kuchunguzwa na hayajawa hitimisho la kisheria kwamba Omar alifanya ulaghai wa uhamiaji. Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani imesema kwa ujumla kwamba haiwezi kutoa maelezo kuhusu uchunguzi unaoendelea, huku ikisisitiza kuwa hakuna mtu, hata Mbunge, aliye juu ya sheria.
Ufafanuzi wa sakata hili ili uelewe zaidi ni kwamba Ilham Omar anasumbuliwa na upinzani wake kisiasa kutokana na mafanikio yake aliyoyapata. Pia ni historia yake ya ndoa ambapo inaonekana kuna mkanganyiko kidogo, kwa sababu zifuatazo:
1. Ilham Omar aliolewa na Ahmed Abdisalan Hirsi (ndoa ya kitamaduni/au kiislamu) 2002 huku ndoa ya kisheria ikifungwa 2009. Wamefanikiwa kupata Watoto 3 nae. Mmoja ni Isra Hirsi ambaye Mwanaharakati kisha wakatengana 2017.
2. Mwaka huohuo (2009), Ilham Omar akafunga ndoa (kiserikali) na Ahmed Nur Said Elmi na waliachana mwaka 2017 ila hawakufanikiwa kupata Mtoto. Na huyu ndiye anayedaiwa kuwa ni Ndugu wa Ilham Omar.
3. Mwaka 2020, Ilham Omar akaolewa na Tim Mynett na ndiye aliyenae hadi sasa lakini hawajafanikiwa kupata Mtoto.
- Kwa nini kunakuwa na mkanganyiko?
Kipindi cha 2009-2011 ndicho kinachozua maswali. Kwa nyaraka za kisheria alionyesha kuwa ameolewa na Elmi, lakini kwa hadharani alikuwa anaishi na Hirsi ambaye ndiye Baba wa Watoto wake watatu.
Yeye mwenyewe amesema alikuwa ametengana na Hirsi kisha akarudiana naye baadaye, na ndoa na Elmi ilikuwa "imani tu" sio ya mapenzi.
#UbuMedia
