Bilionea Aliko Dangote katika mahojiano na Arise News, alipoulizwa kama bado angependa Kuwa na mtoto wa kiume ili aje kuendeleza jina/urithi wa familia, alijibu kuwa siyo kipaumbele chake kuwa na mtoto wa kiume, akieleza kuwa anajivunia mabinti wake watatu na hatua za maendeleo walizofikia.
Aliko Dangote, ambaye ni mfanyabiashara na mwekezaji mwenye mafanikio, alisema unaweza kumuomba Mungu upate mtoto wa kiume, ila akaja kuwa sababu ya anguko la urithi wa familia. Amesema wakati mwingine, kama Mungu hajakupa kitu fulani, shukuru badala ya kulazimisha kuwa nacho.
Dangote amefunguka kuwa haaamini kwamba kama angekuwa na mtoto wa kiume angeleta matokeo mazuri zaidi kuliko yaliyoletwa na mabinti zake watatu.
Watoto wake watatu wa kike, Fatima, Mariya na Halima, ni wasomi wenye taaluma mbalimbali na uzoefu katika biashara na tayari wanafanya kazi katika makampuni ya baba yao. Dangote pia alieleza kuwa anaamini mmoja au wawili kati ya mabinti wake hao watakuja kuongoza Dangote Group.
