WAHAMIAJI HARAMU 197 WAKAMATWA DAR ES SALAAM
Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imekamata jumla ya wahamiaji haramu 197 raia wa Malawi na Burundi, katika misako na doria zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.
Wahamiaji hao wamekamatwa katika kipindi cha kuanzia tarehe 04 hadi 14 Septemba 2026, ambapo kati yao 102 ni raia wa Malawi na 95 ni raia wa Burundi.
Misako hiyo imefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo Mwananyamala, Mbezi kwa Kakobe na Tandale wilayani Kinondoni; Keko, Mbagala na Tandika wilayani Temeke; pamoja na Ubungo na Kigamboni.
Akitoa maelekezo kwa Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Uhamiaji wanaoshiriki katika operesheni za ukamataji na upelelezi wa kesi, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam (SACI), Vincent Haule, amewataka kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo na kwa kuzingatia misingi ya sheria.
SACI Haule pia amezipongeza Ofisi za Uhamiaji za Wilaya za Kinondoni, Temeke, Ilala, Kigamboni na Ubungo kwa juhudi wanazochukua katika kukabiliana na changamoto za uhamiaji usio wa kisheria.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kampeni ya “Mjue Jirani Yako”, inayolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya uhamiaji, ikiwemo umuhimu wa kutoa taarifa kuhusu watu wanaoingia au kuishi nchini bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema elimu hiyo imeendelea kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali katika juhudi za kudhibiti uhamiaji usio wa kisheria na kuimarisha usalama wa jamii.
Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhamiaji usio wa kisheria, huku wakihakikisha taarifa hizo zinawasilishwa kupitia njia rasmi na salama.
