Mkandarasi anaetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 Manyoni ametakiwa kuhakikisha ndani ya siku 30 awe amekabidhi Mradi ukiwa umekamilika na wananchi wa Mji wa Manyoni waanze kupata maji.
Waziri wa Maji Mh. Jumaa Aweso (Mb) ametoa maagizo hayo wakati akikagua maendeleo ya mradi huo wa maji wa Miji 28 katika mji wa Manyoni ,Mkoani Singida.
Mradi wa Maji wa Miji 28 Manyoni unagharimu fedha kiasi cha shilingi bilioni 28 mpaka kukamilika kwakwe ambapo utakua na uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha Lita milioni 6 kwa siku, huku mahitaji ya sasa ya maji ya mji wa Manyoni ni Lita milioni 2 kwa siku.
"Nakupa siku 30 kuanzia hii Leo, hakikisha hadi tarehe 15 oktoba uwe umekabidhi mradi ukiwa umekamilika, hauna kisingizio, fedha zipo vifaa vipo kwaiyo hauna kisingizio chochote, wananchi wa Manyoni wapate maji" Amesema Aweso
Mhe. Aweso pia amepiga marufuku kwa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira Manyoni na Mamlaka zote nchini kuwabambikia bili za maji wananchi na kuzitaka Mamlaka hizo kuhakikisha wananchi wanalipa sawa na walichotumia.
" Niiitake Mamlaka ya Majisafi Manyoni na Mamlaka zote za Maji nchini marufuku kuwabambikia bili wananchi, kwasasa serikali inawekeza katika mita za malipo ya kabla ili wananchi aweze kulipia kiwango anachotaka kukitumia."
Amesema Aweso.
Akimkaribisha Waziri wa Maji, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mh. Vicent ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi nzuri ya kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata maji, akisema kwa Wilaya ya Manyoni yenye vijiji 58 ni Vijiji 7 pekee bado havijapata miundombinu ya maji na anaiona juhudi ya Waziri Aweso katika kuhakikisha vijiji vilivobaki vinapata maji.
