Bodi ya Filamu Tanzania imemfungia Bi. Mwanaharusi Ally Makwinjo kufanya shughuli za filamu na michezo ya kuigiza kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Septemba 15, 2026.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Bodi kufanya kikao cha maadili na Mwanaharusi kufuatia tukio la ukiukwaji wa maadili lililodaiwa kutokea wakati wa maandalizi ya utayarishaji wa filamu katika eneo la Chanika, Dar es Salaam.
Bodi imesema imefikia uamuzi huo baada ya kupitia na kujadili suala hilo kwa kina, huku ikiendelea kuwafuatilia wahusika wengine waliohusishwa na tukio hilo ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa taratibu zinazosimamia tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini.
Bodi ya Filamu Tanzania imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua dhidi ya wadau wa tasnia watakaobainika kwenda kinyume na maadili.
