WASHINGTON — Utawala wa Rais Donald Trump unajiandaa kuidhinisha mauzo ya mabomu mazito 40,000 kwa Israel yenye thamani ya takribani dola bilioni 2.8, kwa mujibu wa The Washington Post.
Mpango huo unahusisha mabomu ya pauni 2,000 aina ya MK-84 na BLU-117, na unatajwa kuwa miongoni mwa mauzo makubwa zaidi ya silaha za aina hiyo kwa Israel katika miaka ya hivi karibuni. Fedha za msaada wa Marekani kwa Israel zinatarajiwa kutumika kugharamia ununuzi huo.
Baadhi ya mabomu hayo ni ya aina ambayo utawala wa Rais wa zamani Joe Biden uliwahi kusitisha usafirishaji wake kwa muda kutokana na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kusababisha vifo vya raia.
Mpango huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge la Marekani (Congress) kwa ajili ya mchakato wa kuidhinishwa. Hatua hiyo inaweza kuzua mjadala mpya kuhusu msaada wa kijeshi kwa Israel, baada ya zaidi ya wabunge 100 wa Democratic katika Baraza la Wawakilishi kupiga kura mwezi Julai kuunga mkono kupunguzwa kwa baadhi ya misaada kwa Israel.
#utaridi
