Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Godbless Lema amesema ameahirisha mkutano wake na Waandishi wa Habari uliokuwa ufanyike leo katika Hoteli ya Golden Tulip baada ya kusikiliza hotuba ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika.
Kauli ya Lema inakuja ikiwa ni siku moja baada ya kuiambia AyoTV kwamba leo Septemba 16, 2026 angezungumza na Waandishi wa Habari kuhusu tuhuma za kuhusika na ‘kulamba asali’.
Kupita andiko lake kwenye mtandao wa Kijamii, Lema amesema “nimedumu katika mapambano haya kwa zaidi ya miaka 22, nimeenda lock-up zaidi ya mara 50, nimezunguka Nchi hii usiku na zaidi ya mara tatu, nimewahi kuwa magerezani mara kadhaa, nimekoswa kuuawa zaidi ya mara tatu, na nimewahi kukimbia Nchi,”.
Amesema katika kipindi chote cha mapambano yake ametoa sadaka kubwa, ikiwemo kwa familia yake, akisisitiza kuwa shughuli za kisiasa kwake si ajira, cheo wala njia ya kujitafutia maslahi.
“Kazi hii kwangu si ajira, si cheo, wala si njia ya kujitafutia maslahi, ni huduma, ni wito, ni kama injili ninayoamini na kuitumikia,” amesema.
