Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limesema Mohamed Bakari (28), Mkazi wa Mbwanga, Wilaya ya Mvumi ambaye taarifa zake zilisambaa zikidai ametekwa katika mazingira ya kutatanisha tangu Septemba 17, 2026, hakutekwa bali aliondoka kutokana na madeni yaliyokuwa yakimkabili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 23, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, taarifa za kupotea kwa Mohamed zilitolewa na Mke wake, Elizabert John (24), ambaye alieleza kuwa Mume wake aliondoka nyumbani akisema anakwenda kutafuta fedha za matumizi lakini hakurejea.
Polisi wamesema baada ya kufanya uchunguzi wa awali na kupata taarifa kutoka kwa Ndugu zake, imebainika kuwa Mohamed amepatikana mkoani Shinyanga akiwa mzima na salama, huku sababu iliyomfanya Mohamed kuondoka ni madeni, hivyo alikwenda kutafuta unafuu wa maisha.
Jeshi la Polisi limewataka Wananchi kupuuza taarifa zisizo za kweli zinazohusisha tukio hilo na utekaji, huku likitoa wito kwa Wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu uhalifu na wahalifu.
