Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imempa ushindi Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa kuruhusu baadhi ya mashahidi aliowaomba waitwe mahakamani kwa hati za wito (subpoena) ili kutoa ushahidi katika kesi ya uhaini inayomkabili.
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, baada ya kupitia hoja za pande zote kufuatia pingamizi lililowekwa na Jamhuri.
Kati ya mashahidi 11 waliopendekezwa na Lissu, mahakama imekubali kutolewa kwa hati za wito kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda; Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), CP Ramadhani King’ai; na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillius Wambura.
Jaji Ndunguru amesema mahakama imebaini kuwa ushahidi wa maafisa hao watatu una umuhimu wa moja kwa moja katika shauri hilo la jinai linaloendelea kusikilizwa.
Hata hivyo, mahakama imekataa kutoa hati za wito kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais Philip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Kwa mujibu wa Jaji Ndunguru, mahakama imebaini kuwa ushahidi wa viongozi hao hauhusiani moja kwa moja na hoja za msingi zinazojadiliwa katika mashtaka ya uhaini yanayomkabili Lissu.
