Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Peter Kiariro, mkazi wa Maore wilayani Same, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Bernard Kiluwa, mwenye umri wa miaka 26, mkazi wa Kijiji cha Mheza, wilayani humo.
Tukio hilo limetokea Oktoba 12, 2026, majira ya usiku katika Kitongoji cha Kalemane, Kijiji cha Mheza, ambapo uchunguzi wa awali unaeleza kuwa chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na wivu wa kimapenzi baada ya marehemu kucheza muziki kwa muda mrefu na mke wa mtuhumiwa katika sherehe ya ubarikio iliyofanyika nyumbani kwa Shabani Rajab.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mtuhumiwa alidaiwa kumwomba marehemu waende pembeni kwa ajili ya mazungumzo, lakini baadaye inadaiwa alimshambulia kwa kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa kisu, na kumjeruhi tumboni na kifuani kabla ya kutoroka.
Bernard alipelekwa katika Kituo cha Afya Ndungu kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa huduma. Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji wa mtuhumiwa ili afikishwe mbele ya sheria.
