Mwenyekiti wa Mtaa wa Wangwaray, Kamili Elias, ameongoza vijana zaidi ya 30 kupanda Mlima Kwaraa wilayani Babati, mkoani Manyara, kwa ajili ya kuzima moto uliokuwa ukiteketeza maeneo ya msitu huo, akisisitiza umuhimu wa kulinda misitu kwa manufaa ya jamii.
Elias amesema aliamua kuwahamasisha vijana na wananchi kushiriki katika zoezi hilo kutokana na umuhimu wa msitu huo kwa maisha ya wakazi wa maeneo hayo, ikiwemo uhifadhi wa vyanzo vya maji na upatikanaji wa hewa safi.
Amesema moto huo ulianza Oktoba 25, 2026, na kuteketeza maeneo matatu ambayo ni Mrara, Wangwaray na upande wa Nangara, hali iliyowalazimu wananchi kuungana katika juhudi za kuudhibiti moto huo.
"Tulivyomaliza upande huu wa kwetu tukahamia Mrara na Nangara na kote tulizima moto huo" alisema Mwenyekiti
Mwenyekiti huyo amelaani kitendo cha mtu au watu wanaodhaniwa kuhusika na uchomaji wa msitu huo, akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, ameiomba Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za misitu na madhara yanayotokana na uchomaji holela, ili kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi wa mazingira.
Elias amewashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi la kuzima moto huo pamoja na TFS kwa kuwa karibu nao wakati wa zoezi hilo.
Jitihada hizo zinaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa maeneo, wananchi na taasisi zinazohusika na uhifadhi katika kulinda misitu dhidi ya majanga ya moto.
