Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara limesema limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 10 wa makosa ya mauaji yaliyotokea katika Wilaya ya Simanjiro kwa nyakati tofauti, kuanzia Oktoba 2025 hadi Oktoba 2026.
Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi Oktoba 26, 2026 limeeleza kuwa kati ya watuhumiwa hao, saba tayari wamefikishwa mahakamani, huku upelelezi ukiendelea kwa watuhumiwa wengine watatu.
Watuhumiwa ambao upelelezi wa kesi zao unaendelea ni Emmanuel Paul na Abdalah Mohamed, wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Leonard, mkulima na mkazi wa Mtaa wa Madukani.
Mtuhumiwa mwingine ni Mohamed Juma, anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyakazi wake, Mohamed Kipara, ambaye pia alikuwa mkazi wa Mtaa wa Madukani.
Kwa upande wa watuhumiwa ambao kesi zao zipo mahakamani katika hatua mbalimbali, Jeshi la Polisi limewataja kuwa ni Ambrose Matepeli, Mudi Saidi, Ester Rokoine, Juma Athuman, Revocatus Finias, Juma Sembua na Juma Elifasi.
Ufafanuzi huo umetolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kufuatia taarifa zilizosambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii zikidai kuwa watuhumiwa wa mauaji yaliyotokea Simanjiro hawajakamatwa.
Jeshi hilo limewasihi wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kutoa malalamiko yasiyo na ukweli.
Pia limewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa sahihi za matukio ya uhalifu kwa polisi ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa.
