Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Gift Eliaika, ameagwa. Eliaika aliuawa pamoja na wahifadhi wenzake watano katika shambulio lililotokea wakati wa operesheni ya kukamata mifugo ndani ya eneo la Hifadhi ya Wanyamapori Iswangala wilayani Sikonge, mkoani Tabora.
Katika shughuli hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja mstaafu Hamisi Semfuko, amekemea mauaji hayo na kusema Bodi hiyo haitakubali kitendo hicho, alichokieleza kuwa ni cha kiharamia dhidi ya askari wake.
Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamis Mnanachi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, amesema Serikali inaendelea na uchunguzi kubaini iwapo kweli watu wanaodaiwa kutekeleza shambulio hilo ni wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa katika operesheni hiyo.
Amesema iwapo uchunguzi utabaini wahusika, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika tukio hilo, watu waliotekeleza shambulio hilo wanadaiwa pia kupora silaha aina ya AK-47 mbili na rifle moja, huku silaha nyingine aina ya AK-47 ikichomwa moto pamoja na gari aina ya Toyota Land Cruiser.
Aidha, watu hao wanadaiwa kutokomea na mifugo iliyokuwa imekamatwa katika operesheni hiyo, ambayo wafugaji walitakiwa kulipia faini ya zaidi ya shilingi milioni 100.
Mwili wa Gift Eliaika umesafirishwa kuelekea Arusha kwa ajili ya mazishi, huku miili ya wahifadhi wengine watano waliofariki dunia katika tukio hilo ikizikwa katika maeneo mbalimbali.
