Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wafanyabiashara wadogo wadogo, maarufu kama wamachinga, kutobweteka na kiwango cha biashara walichofikia, bali kuhakikisha wanakua na kujiinua kiuchumi.
Akizungumza na wafanyabiashara katika eneo la Kariakoo, Chalamila amesema ni jambo la kusikitisha kwa mtu kuanza biashara ndogo akiwa na miaka 20 au 25, lakini anapofikisha miaka 40 bado anaendelea kufanya biashara katika kiwango kilekile.
Amesema hali hiyo inaweza kuashiria kuwepo kwa changamoto katika uendeshaji wa biashara, akiwataka wafanyabiashara hao kutumia wataalamu wa masuala ya biashara ili kuwasaidia kukuza shughuli zao.
Pia amewataka wafanyabiashara kutumia maeneo rasmi ya biashara na kuachana na kuweka bidhaa kwenye mitaro au mbele ya maduka ya watu wengine, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha kupata maeneo ya biashara.
