Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, ameripotiwa kutokuwa na mpango wa kufanya kampeni ya hadharani au kujitangaza ili kushinda tuzo ya Ballon d’Or 2026, licha ya kumaliza msimu akiwa na idadi kubwa zaidi ya mabao na pasi za mwisho (Assist) ikilinganishwa na Wachezaji wengine wa tuzo hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu walio karibu na Kane wamesema msimamo huo unaendana na namna ambavyo amekuwa akiendesha maisha yake ya soka kwa muda mrefu, akipa kipaumbele mafanikio ya timu kuliko tuzo binafsi na kuacha kiwango chake uwanjani kijieleze.
Kane anatajwa kujivunia sana kuwa miongoni mwa wanaowania tuzo kubwa zaidi ya mtu binafsi katika soka, lakini hana nia ya kubadili mtazamo wake wa unyenyekevu wala kufanya kampeni hadharani kueleza kwa nini anastahili kushinda.
Badala yake, Straika huyo wa Bayern Munich anaendelea kuelekeza nguvu zake katika kuisaidia klabu hiyo kushinda mataji, huku akiacha wapiga kura kufanya uamuzi wao kuhusu mshindi wa Ballon d’Or 2026.
