Hii Ndio Historia Ya Biblia Takatifu

Baba Abby
0

 



Kabla hujasoma makala hii—ukweli mmoja lazima uwekwe wazi:


​Post hii si shambulio dhidi ya Biblia, wala si jaribio la kutikisa imani yako. Hii ni HISTORIA. Na historia ikisomwa kwa uaminifu na akili iliyowazi, haidhoofishi imani—bali inaijenga kuwa imara zaidi.


​Kwa sababu imani isiyoweza kuvumilia maswali ya kimsingi, haikuwahi kujengwa kwenye mwamba imara.


​Hivyo basi, wacha tuulize maswali ambayo wengi wanaogopa kuyauliza.


​Biblia si kitabu kimoja kilichoshuka kutoka mbinguni siku moja. Ni maktaba ya vitabu 66, vilivyoandikwa kwa zaidi ya miaka 1,000, katika lugha tatu tofauti (Kiebrania, Kiaramu, na Kiyunani/Kigiriki), na zaidi ya waandishi 40 tofauti.


​Waandishi hawa hawakukaa kwenye chumba kimoja kubadilishana mawazo. Walitenganishwa na karne nyingi na mabara mbalimbali. Miongoni mwao alikuwepo mchungaji wa wanyama, mfalme, mvuvi wa samaki, mtoza ushuru, daktari, jenerali wa vita, mfungwa, na mshairi.


​Kila mwandishi alileta lugha yake, utamaduni wake, na mazingira ya zama zake. Barua aliyoandika Mtume Paulo kwa kanisa la Korintho iliandikwa kwa ajili ya matatizo ya Korintho ya miaka 2,000 iliyopita—sio kwa ajili ya waumini wa leo.


​Lakini ajabu kubwa ya kihistoria ni jinsi maktaba hii iliyoandikwa na watu 40 waliotengana kwa karne nyingi inavyobeba ujumbe mmoja unaoshikana kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho.


​Hapa ndipo uaminifu wa kiakili unapohitajika zaidi.


​Watu wengi—wakiongozwa na riwaya maarufu ya The Da Vinci Code ya Dan Brown—yanaamini kuwa Baraza la Nikaea (Council of Nicaea) la mwaka 325 AD, lililoitishwa na Mfalme Constantine wa Roma, ndipo maaskofu walipopiga kura kuchagua vitabu vya kuingia kwenye Biblia na kuvitupa vingine.


​Huo ni uongo wa kihistoria.


​Hakuna kumbukumbu yoyote ya kihistoria inayothibitisha kuwa Baraza la Nikaea lilijadili au kuchagua vitabu vya Biblia. Lengo kuu la Nikaea lilikuwa ni mjadala wa kiteolojia kuhusu asili ya Yesu—sio kuchagua maandiko.


​Kuundwa kwa Biblia haikuwa kura ya siku moja kwenye chumba cha mfalme. Ulikuwa ni mchakato wa karne nyingi wa makanisa ya kale kukubaliana kwa pamoja ni maandiko gani yalikuwa na mamlaka ya kitume.


​Vigezo vitatu vilitumika:


​Uhusiano wa Kitume: Je, kiliandikwa na Mtume au mtu aliyekuwa karibu na Mitume?


​Uwiano wa Mafundisho: Je, kinafundisha mtazamo unaoendana na mafundisho makuu ya Ukristo?


​Kukubalika kwa Jamii: Je, kilikuwa kinatumiwa na kukubalika kwa upana na makanisa mengi ya kale?


​Mchakato huu ulikuwa na migogoro mikubwa. Vitabu kama Ufunuo na Waebrania vilijadiliwa kwa karne nyingi kabla ya kukubalika. Hadi kufikia mwishoni mwa karne ya 4—kwenye Mabaraza ya Hippo (393 AD) na Carthage (397 AD)—ndipo orodha rasmi (Canon) ya Agano Jipya ilipothibitishwa.


​Mfalme Constantine hakuchagua vitabu vya Biblia, lakini kugeukia kwake Ukristo mwaka 313 AD kubadilisha kila kitu.


​Wakati Ukristo ulipofanywa kuwa dini rasmi ya Dola ya Roma, himaya ilihitaji kitu kimoja: Umoja na Udhibiti. Dola kubwa kama Roma isingeweza kuendeshwa na mtandao wa makanisa yenye mafundisho yanayopingana. Roma ilihitaji Kanisa Moja, Msimamo Mmoja, na Biblia Moja.


​Hapo ndipo vitabu vingine kama Injili ya Tomaso, Injili ya Filipo, na Kitabu cha Henoko (Hiki makala yake nimekwisha iandaa) vilipopigwa marufuku na kutangazwa kuwa vya uzushi.


​Ni lazima ujiulize swali hili zito la kihistoria:


​Ni nini kinatokea wakati imani iliyoanzia chini kama harakati ya mafukara, waliokandamizwa, na waliotengwa na jamii, inapochukuliwa na kuwa dini rasmi ya Dola ya Kijeshi yenye nguvu zaidi duniani?


​Je, Biblia iliyotoka kwenye mchakato huo inabeba picha nzima ya ukweli wa kiroho, au inabeba picha ambayo Dola ya Roma iliona inafaa zaidi kwa ajili ya kutawalia watu?


​Hii inaleta maswali mawili ya kutafakari:


​Je, unaamini kuwa mchakato wa kuchuja vitabu vya Biblia uliongozwa na ufunuo wa Mungu tu, au uliingiliwa na maslahi ya kisiasa ya Dola ya Roma?


​Kama ungegundua kuwa vitabu vilivyotupwa nje (kama Book of Enoch au Gospel of Thomas) vina taarifa za kweli za kihistoria, je, ungekuwa tayari kuvisoma na kuviamini kama sehemu ya maarifa yako?

Tags

Post a Comment

0 Comments

Post a Comment (0)

#buttons=(Ok, Go it!) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Check Now
Ok, Go it!