Katibu wa Idara ya Organaizesheni ya CCM, Paul Chacha, ameibua mjadala baada ya kusema kuwa viongozi wa Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ni “vyetu”, akirejea mfumo wa CCM uliowaweka viongozi hao madarakani.
Chacha alitoa kauli hiyo Septemba 26, 2026, wakati akihutubia Mkutano uliokuwa na lengo la kutathmini hali ya kisiasa na kuandaa mikakati ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa CCM wa mwaka 2027, pamoja na maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya chama hicho.
Katika hotuba yake, Chacha alisisitiza kuwa mfumo mzima wa kiutendaji wa serikali na vyombo vya dola unapaswa kukitumikia chama tawala kwa kuwa ndicho kilichoweka viongozi hao madarakani.
"Vyombo vyote hivi ni vyetu, viongozi wote ni wetu kwa sababu mfumo wa CCM ndio uliowaweka hapo," alisema Chacha wakati akifafanua ushawishi na nguvu ya chama hicho kuelekea chaguzi zijazo.
Kauli hiyo imeibua mjadala kwenye mitandao na miongoni mwa wadau wa siasa kuhusu nafasi ya vyombo vya dola katika mfumo wa vyama vingi, huku wakosoaji wakisema taasisi hizo zinapaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na sheria, bila kujali chama cha mtu.
